AJTC VOICE FO VOICLESS

Jumatatu, 19 Desemba 2016

habari za jumatatu

 

 Monday, December 19, 2016


Rais Magufuli Afanya Uteuzi Wa Wakuu Wa Wilaya Wawili Na Wakurugenzi Watatu .........Nafasi ya Humphrey Polepole yachukuliwa na Kisare Makori


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 19 Desemba, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi 3 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Kisare M. Makori kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Bw. Kisare M. Makori anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Humphrey Polepole ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Avod Mmanda Herman kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara iliyopo katika Mkoa wa Mtwara.

Bw. Avod Mmanda Herman anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Khatib M. Kazungu ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Ramadhan Geodrey Mwangulumbi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga iliyopo Mkoani Shinyanga.

Bw. Ramadhan Geodrey Mwangulumbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Lewis Kalinjuna ambaye anastaafu kwa mujibu wa Sheria.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw Rojas John Romuli kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda iliyopo katika Mkoa wa Katavi.

Bw. Rojas John Romuli anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ngalinda Hawamu Ahmada aliyefariki dunia hivi karibuni.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Rashid K. Gembe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga iliyopo katika Mkoa wa Tanga.

Bw. Rashid K. Gembe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Mkumbo Emmanuel Barnabas ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni.

Uteuzi wa huu unaanza mara moja na wateule wote wanatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mara wapatapo taarifa hii.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

19 Desemba, 2016

Monday, December 19, 2016

Wananchi 21 wafikishwa mahakamani kwa kuvamia na kufanya vurugu katika kituo cha polisi.

Jumla ya watuhumiwa 21 akiwemo mwanamke mmoja wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Chunya kwa kuhusika na vurugu zilizotokana na wananchi wilayani humo kuvamia kituo cha polisi kwa lengo la kuwatoa watuhumiwa wa mauaji ili kuwaadhibu.

Watu hao waliofikishwa mahakamani ni sehemu ya watuhumiwa 41 waliokamatwa, kati yao wanaume wakiwa 34 na wanaweke 7 baada ya vurugu zilizotokea jana na kusabababisha jumla ya watu 7 kujeruhiwa wakiwemo askari polisi wanne, na wananchi watatu huku mwananchi mmoja aliyefahamika kwa jina la AMOKE MBILINYI (25) akifariki dunia.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya imeeleza kuwa tukio hilo limetokea mnamo tarehe 18.12.2016 majira ya saa 11:45 asubuhi katika Kituo cha Polisi Makongolosi kilichopo Kata ya Makongolisi, Wilayani Chunya ambapo kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi walivamia kituo hicho cha Polisi na kufanya fujo kwa kuwarushia  mawe hovyo askari.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, lengo la uvamizi huo ilikuwa ni kuwatoa watuhumiwa wawili waliofahamika kwa majina ya 1. ERASTO ROBERT, mkazi wa Kilombero na 2. BASI LINUS mkazi wa Makongolosi waliokuwa wanakabiliwa na kosa la mauaji kwa lengo la kuwatoa nje na kuwauawa kwa kuwachoma moto. 

Aidha wananchi hao walifunga barabara ya Chunya/Makongolosi kwa kuweka mawe makubwa na magogo hali iliyosababisha usumbufu mkubwa wa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Jeshi hilo limesema thamani ya uharibifu bado kufahamika na hali imerejea kuwa shwari

Awali mnamo tarehe 11.12.2016 majira ya saa 23:20 katika Kitongoji cha Manyanya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JACOB BROWN Mkazi wa Manyanya alivamiwa na watu wasiojulikana akiwa peke yake shambani kwake na kuuawa ambapo Polisi walifanya msako na kuwakamata watu hao wawili kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
 

Monday, December 19, 2016

Uteuzi: Rais Dkt Magufuli ateua Wenyeviti 7 wa Bodi za Taasisi za Serikali


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amefanya uteuzi wa Wenyeviti 7 wa Bodi za Taasisi za Serikali, na pia ameteua Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania na Mjumbe mmoja wa Baraza la Taifa la Biashara.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 19 Desemba, 2016 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imewataja walioteuliwa kama ifuatavyo;
 
1. Rais Magufuli amemteua Bw. Ali Mufuruki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira.
 
Ali Mufuruki ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Infotech Investment na Mwenyekiti wa Taasisi ya Afrika inayojihusisha na uendelezaji wa vipaji vya uongozi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 
2. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Christopher Kajolo Chiza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade)
Mhandisi Christopher Kajolo Chiza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Sabetha Mwambenja ambaye amemaliza muda wake.
 
3. Rais Magufuli amemteua Bw. Peter M. Maduki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
 
Peter M. Maduki anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Idrissa Mshoro ambaye amemaliza muda wake.
 
4. Rais Magufuli amemteua Dkt. Yamungu Kayandabila kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
 
Dkt. Yamungu Kayandabila ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Peter Ilomo ambaye amemaliza muda wake.
 
5. Rais Magufuli amemteua Prof. Godwin Daniel Mjema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Fedha na Mikopo (UTT-MFI)
 
Prof. Godwin Daniel Mjema ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Fadhili D. Mbaga ambaye amemaliza muda wake.
 
6. Rais Magufuli amemteua Kepteni Ernest Mihayo Bupamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Bahari (DMI)
 
Kepteni Ernest Mihayo Bupamba ni Mwendesha Meli Mkuu (Principal Captain) Katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
 
7. Rais Magufuli amemteua Dkt. Aloyce S. Hepelwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID)
 
Dkt. Aloyce S. Hepewa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. John Jingu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Tanzania.
 
Dkt. John Jingu ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Halikadhalika, Rais Magufuli amemteua Dkt. Rashid Adam Tamatama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI).
 
 Dkt. Rashid Adam Tamatama ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
 
Pia, Rais Magufuli amemteua Bibi. Zuhura Muro kuwa Mjumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Council – TNBC).
 
Bibi. Zuhura Muro ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojihusisha na huduma za ushauri wa ubora na mafunzo (Service Limited) katika ofisi zake za Dar es Salaam.
 
 Wateule wote waliotajwa hapo juu, uteuzi wao umeanza tarehe 17 Desemba, 2016
 
 Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Desemba, 2016

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni