AJTC VOICE FO VOICLESS

Ijumaa, 23 Desemba 2016

habari za leo hii

Saturday, December 24, 2016

Mbowe Aeleza kwa nini Amekuwa Kimya Kupotea kwa Ben Saanane

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi. 

Mbowe alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa. 

Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake. 

“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema Mbowe. 

Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.” 

Katika hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba imeendelea kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo mahabusu. Alisema hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani. 

Akijibu madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa mbalimbali vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi haimkamati mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha sheria. 

“Hayo yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi. Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa mjomba wangu tutamkamata.” 

Msigwa kidedea 
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliibuka kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na asilimia 58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa. 

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na asilimia 88 ya kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika. 
Mnyika alisema kuwa nafasi ya  mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa. 

Mnyika alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au hapana kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa kuweka wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya chama. 

“Hivyo Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea wote na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo" Alisema Mnyika

Saturday, December 24, 2016


Kingunge Asema Bila tume huru Wapinzani Wasahau Kuingia Ikulu .......Lowassa Akubali Yaliyopita Si Ndwele

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.

Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.

Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi wake kote nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.

Kingunge, aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.

“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.

Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana.”

Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.

“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.

Alisema enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga na Tanu kupigania uhuru.

“Tulifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,” alisema.

“Ninyi mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”

Akizungumza mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.

“Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa. 

Saturday, December 24, 2016


Penzi la Bibi wa Miaka 60 Laua Kijana wa Miaka 23



KIJANA mwenye umri wa 23 na mpenzi wake, bibi mwenye umri wa miaka 60 , wakazi wa kijiji cha Tentula, Kata ya Ikozi wilayani Sumbawanga, wanashikiliwa na polisi wakihutumiwa kumshambulia na kumuua kikatili jirani yao aitwae Desder Justino (23) kwa kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Inaelezwa kuwa, Justino pia alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na bibi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mauaji hayo yalitokea Desemba 21 mwaka huu saa nne asubuhi katika nyumba ya mwanamke huyo iliyopo kijijini Tentula.

Taarifa kutoka kijijini humo zinadai kuwa, mwanamke huyo licha ya umri wake kuwa mkubwa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na vijana hao wawili wa rika moja.

Kamanda Kyando hakuwa tayari kutaja majina ya wapenzi hao ambao ni watuhumiwa wa mauaji kwa sababu za uchunguzi.

Lakini alisema mwanaume ana umri wa miaka 23 huku mpenzi wake ana umri wa miaka 60. Akielezea zaidi, Kamanda Kyando alisema siku ya tukio Justino alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi na kumkuta kijana mwingine (mtuhumiwa), na hapo ndipo ugomvi ukaibuka baina ya vijana hao.Alisema Justino alijeruwa kichwani.

“Wawili hao yaani wapenzi hao (mwanamke na mwanaume) walimshambulia Justino (Desder) kwa kumpiga kichwani na kitu chenye ncha kali na kumjeruhi vibaya na alikufa akiwa anatibiwa hospitalini,” alisema Kamanda Kyando na kuongeza  kuwa, watuhumiwa hao wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi wa awali utakapokamilika.


Saturday, December 24, 2016


Makamu wa Rais ataka wazazi na walezi kuacha kuwaoza watoto wakiwa wadogo



MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi wa visiwani Zanzibar, kuacha tabia ya kuwaoza wasichana wakiwa na umri mdogo, bali wawasomeshe kwa ajili ya manufaa yao ya jamii kwa ujumla.

Samia alisema hayo kwa nyakati tofauti, wakati akizindua madarasa ya kisasa iliyojengwa kwenye eneo la Kilimani na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote nchini Tanzania unaojengwa katika eneo la Ijitimai Kidoti mkoani Kaskazini Unguja.

Ujenzi huo unafanywa kwa michango ya wananchi. Alisema hayo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Unguja.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar, ilieleza kuwa makamu huyo wa Rais yupo katika ziara visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Samia alisema kama wazazi na walezi watasomesha watoto wa kike, elimu watakayopata itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana hao, kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika jamii.

Alisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa mtoto wa kike, hivyo ni muhimu kwa jamii ya Zanzibar ihakikishe watoto wa kike wote wanapata elimu, kwani watakuwa na uwezo wa kuchagua na kuandaa mustakbali wa maisha yao ya baadaye, ikilinganishwa na hali ilivyo sasa kwenye baadhi ya maeneo.

Kuhusu elimu ya dini, aliwahimiza wazazi na walezi, kuwalea watoto katika maadili mema kwa kuzingatia maandiko matakatifu ya Mtume Mohammad (S.A.W).



aturday, December 24, 2016


Jaji Magimbi kusikiliza rufaa ya Godbless Lema Desemba 28



JAJI Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa ya kutaka dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Desemba 28 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016, imepangiwa kusikilizwa na Jaji huyo. Alisema kimsingi wanalalamikia uamuzi wa Mahakama kutomwachia huru, licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpatia dhamana.

Awali, uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, uliweka wazi dhamana.

Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai kuwa sheria haizuii kumpa dhamana mtu kwa kesi ya uchochezi, ila kabla ya kutoa masharti ya dhamana licha ya kutamka dhamana ipo wazi, mawakili wa serikali walipinga kumpatia dhamana Lema, kwa madai wameonesha nia ya kukata rufaa.

Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo na mtuhumiwa asubiri maamuzi ya Mahakama Kuu.

Lema alilazimika kwenda mahabusu hadi sasa katika Gereza Kuu la Kisongo. Baada ya hatua hiyo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck Mfinanga, walianza kutafuta suluhisho la mteja wao kupata dhamana na walianza na kuandika maombi na kuitaka Mahakama Kuu kufanya marejeo kwa kuitisha faili la kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Lakini, ombi lilitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu kwa madai kuwa walikosea, badala ya kufanya marejeo walitakiwa kukata rufaa. Mawakili hao walilazimika kukata rufaa siku hiyo hiyo na Desemba 2 mwaka huu, ilitupwa na Jaji Fatuma Masengi kwa madai kuwa ilikuwa nje ya muda.

Baada ya hatua hiyo, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufaa yao juu ya dhamana na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk Modesta Opiyo, alikubali na kumwongezea muda Lema wa siku 10.

Siku hiyo ya kuongezewa muda, mawakili wa Lema walifanikiwa kukata rufaa hiyo. Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi katika mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo.

Alikamatwa Novemba 2 mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba nane mwaka huu, akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni