STAND UNITED WATAKA BARUA YA MAHAKAMA ILI KUMUACHIA OWINO UARABUNI
Klabu
ya Stand United ya Shinyanga imesema imechezwa na ‘machale’ ya kuwepo
mchezo mchafu unaotaka kuchezwa na beki wao, Joseph Owino ambaye amekuwa
akishinikiza apewe barua ya kuachwa, lakini ili kukwepa kesi wamemtaka
aje na barua iliyosainiwa na hakimu ndipo wampe barua ya kumuacha
‘release letter’.
Owino
hana maelewano mazuri na viongozi wake tangu abaniwe kujiunga na Fanja
ya Oman ambayo ilikubaliwa kumchukua lakini ikashindwa kutimiza masharti
ya Stand, ikiwemo kutuma kwanza fedha za kumununua kabla ya kupewa
barua ya kumuacha lakini wakakataa.
Tangu kipindi hicho, Owino amekuwa kwenye msigano na uongozi wa Stand huku akibembeleza aachwe huru.
Katibu
wa Stand, Kennedy Nyangi ameliambia Championi Ijumaa kuwa wamefikia
wazo hilo kutokana na ukweli Owino anawadai fedha ya usajili, hivyo
kumpa barua ya kumuacha ni njia ya kuwafungulia kesi.
“Siyo
yeye tu, wachezaji wote waliosajiliwa msimu huu hakuna ambaye
ameishapata fedha za usajili, lakini mwenyewe amezidi kutushinikiza
tumpe barua ya kumuacha na kwamba atasamehe kila kitu.
“Tumemweleza
kama amedhamiria kweli, basi atuandikie barua iliyosainiwa na hakimu
kuthibitisha kwamba anaondoka kiroho safi, siyo tumpe barua halafu kesho
atufungulie mashtaka, hilo hatutaki,” alisema Nyangi.
ILE ISHU YA MKUDE KUWAZIMIA SIMBA SIMU IKO NAMNA HII....
Hakika unaweza kushangazwa na namna
Simba inavyohaha kuwabakiza vijana iliowalea na taarifa zinasema kijana
aliyepewa unahodha, Jonas Mkude amewazimia simu viongozi wa klabu hiyo.
Habari za uhakika zinasema, Simba
wamekuwa wakihaha kumpata Mkude ili kumalizana naye katika suala la
usajili, lakini yeye alikuwa amezima simu tangu Jumatatu.
“Kweli Mkude alizima simu kabisa baada
ya kuwa tumefanya naye majadiliano kwa mara ya kwanza. Kukawa hakuna
mwafaka sahihi, wakati tunasubiri arudi kumalizana naye, akazima simu.
“Tulimtafuta kwa siku mbili, mwisho
tukawaambia Meneja Mussa Mgosi na Mratibu, Abbas Ally kumtafuta. Nao
wakafanya hivyo bila ya mafanikio na mwisho tumeamua kukaa kimya na
kusubiri,” chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kilieleza.
“Sasa kama anataka kusaini sawa, au
tumesikia kuna mtu kamshawishi asisaini ili akacheze Afrika Kusini sawa.
Tunajua namna ya kulifanyia kazi hili na kupata jibu. Tumechoka
kufanywa kama watoto.”
Imeelezwa, ili kuongeza mkataba Mkude
alikuwa akitaka kupewa Sh milioni 80, baadaye akashuka hadi 60 wakati
Simba walikuwa wameishia 40, wakapanda hadi 50 na Mkude ndiyo akaamua
kuzima simu.
Wiki hii mwanzoni, Mkude aliliambia
gazeti hili atakwenda kusaini Yanga badala ya Simba kama hali ya
kutofikia mwafaka itaendelea.
Lakini siku chache baadaye, Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye akatoa kauli yake kwamba hawana
mpango na Mkude na wanaangalia mbali zaidi kwa kusaka viungo ‘wakata
umeme’ wenye uzoefu kwa ajili ya michuano ya kimataifa na inaelezwa hiyo
inaweza ikawa sababu ya kumtia hofu Mkude na huenda akaanza kuwatafuta
viongozi wa Simba, ili wamalizane.
Inaripotiwa kuwa juzi na jana Mkude
alikuwa mmoja wa wachezaji wa Simba walioshiriki katika mazoezi ya timu
hiyo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi jijini Dar.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni